Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Zanzibar na Kitengo cha Elimu ya Juu kuandaa kongamano na kuwaita vijana wanaomaliza kidato cha sita ili kutoa fursa zinazotoka katika Vyuo Vikuu nchini. Agizo hilo amelitoa wakati akifunga maonesho wiki ya Elimu ya Juu katika Mnara wa Mapinduzi Square Michenzani Mjini Unguja. Amesema hatua hiyo itawawezesha vijana kujua fursa zinazopatikana katika Vyuo vikuu na fani ambazo zina tija kwa nchi yao na zitakazowawezesha kujiajiri. Amesema ni vyema kuhakikisha wanakaa pamoja katika kuratibu kongamano hilo kwa ajili ya kuwawezesha Wanafunzi kupata uelewa na taaluma juu ya fursa zilizokuwepo katika vyuo Vikuu nchini. Naibu Gulam amewapongeza washiriki wa maonesho kwa kuamua kutoa huduma zao ili kuonesha fani na mambo mbalimbali yanayotolewa katika vyuo vyao kwani wametimiza azma ya Serikali kwa kutoa huduma kwa wanafunzi kwa ajili ya kujiandaa ili waweze kuchagua fani ambazo wanataka kujiunga na vyuo vikuu. Hata hivyo amebainisha kwamba katika wiki hiyo anaamini vyuo vimefaidika na kuamini dhamira na lengo lilokusudiwa limefikiwa kwa asilimia kubwa. Amewashauri vijana kuendelea kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kuona fursa mbalimbali watakazoweza kuzitumia na kuahidi kwamba Wizara itaendelea kutoa ushirikiano wakati wote katika sekta hiyo muhimu ya elimu. Mbali na hayo ameahidi kufanya ziara katika vyuo vikuu vilivyokuwepo nchini ili kuona changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuboresha elimu ya juu katika nchi. Pia ametoa ushauri kwa Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Juu katika maonesho yanayokuja kuhakikisha anashirikisha wakuu wa vyuo tofauti ili kuonesha changamoto zilizojitokeza katika maonesho hayo na kuweza kuzikabili na zisiweze kujitokeza tena katika maonesho hayo. “Zipo changamoto ambazo zimejitokeza katika maonesho haya ikiwemo ufinyu wa nafasi , pamoja na kuona changamoto hii mnaiondosha kwani lengo letu ni kuona vyuo vingi viweze kushiriki ili kuwapa vijana taaluma wakati wanapotaka kujiunga na vyuo,” amesisitiza. Aidha ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha wananchi na wanafunzi kushiriki katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu kwani sensa ina umuhimu kwa Serikali na Wizara kwa ujumla katika kuiwezesha serikali kujua mahitaji ya wananchi. Sambamba na hayo amesisitiza suala la kutunza amani na utulivu wa nchi ili kuiwezesha Serikali kuendelea kuleta maendeleo wanayoyatarajia. Nae Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Elimu ya Juu, bi Aida Juma Maoulid amesema maonesho hayo yanaimarisha udugu kwa sekta za elimu ya juu nchini na anaamini wanaodoka katika maonesho hayo kwenda kuongeza nguvu katika sekta hiyo. Akitoa shukurani kwa niaba ya washiriki wa maonesho hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA, Professa Mohammed Makame, amesema wanatambua juhudi zinazotolewa na Wizara na wamewaongezea juhudi za kushiriki maonesho hayo ya wiki ya elimu ya juu Zanzibar katika kutambulisha fursa zilizokuwepo katika Vyuo vyao. Amesema wiki hiyo ina manufaa kwao katika kuwakutanisha wanataaluma na wadau wengine wa walimu wakiwemo wazee na Wanafunzi kuendeleza maendeleo bora ya elimu ya juu ndani ya nchi. Amesisitiza wazo la kupata eneo kubwa zaidi katika kuona maonesho yanayokuja wanaongeza idadi ya washiriki.