Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Ali Abdulgulam Hussein amewataka walimu watakaosimamia zoezi la ugawaji wa madaftari kuhakikisha wanatimiza malengo ya serikali ya kutoa elimu bila ya malipo. Amesema hayo wakati wa zoezi la ugawaji wa madaftari kwa ajili ya wanafunzi wa skuli za maandalizi na msingi mkoa wa mjini magharibi huko Mazizini Unguja. Amesema lengo la serikali ni kuendeleza utaratibu wa wananchi kupata elimu bure. Amesema ili elimu ipatikane kwa Kiwango bora zaidi ni vyema kuendelea kuimarisha zaidi ili taifa kizalishe wataalamu wazalendo. Akizungumza suala la kuchelewa kwa madaftari hayo amesema ni kutokana na kutafuta kiwanda chenya kuzalisha madaftari yenye kiwango kizuri zaidi. Nae Mkurugenzi idara ya maandalizi na msingi wizara ya elimu bi Fatma Mode Ramadhan amesema zoezi hilo ni endelevu kwa Zanzibar ili kuhakikisha wanafunzi wote wa msingi na maandalizi wananufaika na madaftar hayo. Kwa upande wao walimu wakuu wa skuli za Mkoa wa Mjini Magharibi waliopokea madaftari hayo wameipongeza serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuhakikisha wanafanyia kazi kilio chao cha muda mrefu ili kuhakikisha sekta ya elimu inaendelea kupiga hatua nchini. Jumla ya wanafunzi laki 314,672 wa msingi na elfu 61,951 kwa maandalizi na vituo vya tutu watanufaika na madaftari hayo.