Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki dunia. Habari hizo zimethibitishwa leo na Rais wa Zanzibar, Dokta Hussein Ali Mwinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani humo. Akitowa tangazo la kifo hicho mchana huu, Rais Mwinyi amesema makamu wake huyo wa kwanza amefariki dunia saa tano asubuhi ya leo wakati akitibiwa jijini Dar es Salaam. Bila ya kutaja ugonjwa uliokuwa ukimsibu, rais huyo ametowa mkono wa pole kwa Wazanzibari na Watanzania wote. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amesema ameshtushwa na kifo cha Maalim Seif. Katika ukurasa wake wa Twitter, Rais Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Mwinyi, familia ya Seif, Wazanzibari, wnachama wa ACT-Wazalendo pamoja na Watanzania wote kwa ujumla. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad anatarajiwa kuzikwa kesho 18/02/2021 huko kijijini kwao Nyali Mtambwe Mkoa wa Kaskazini Pemba. Mungu Ailaze Roho ya marehemu Mahali Pema Peponi, Ameen.